Zaburi Sura 146
1
Haleluya.
2
Nitamsifu Bwana muda ninaoishi, Nitamwimbia Mungu wangu ningali ni hai.
3
Msiwatumainie wakuu, Wala binadamu ambaye hakuna wokovu kwake.
4
Pumzi yake hutoka, huurudia udongo wake, Siku hiyo mawazo yake yapotea.
5
Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake, Na tumaini lake ni kwa Bwana, Mungu wake,
6
Aliyezifanya mbingu na nchi, Bahari na vitu vyote vilivyomo. Huishika kweli milele,
7
Huwafanyia hukumu walioonewa, Huwapa wenye njaa chakula; Bwana hufungua waliofungwa;
8
Bwana huwafumbua macho waliopofuka; Bwana huwainua walioinama; Bwana huwapenda wenye haki;
9
Bwana huwahifadhi wageni; Huwategemeza yatima na mjane; Bali njia ya wasio haki huipotosha.
10
Bwana atamiliki milele, Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. Haleluya.